Kilio Changu Mwajiriwa


Jeph International2022/05/22 14:17
Follow
Kilio Changu Mwajiriwa

Kwa kweli nina hasira, kwa yale unayotenda

Wewe ulo na ajira, mesahau ya kalenda

Wanipa chache mshara, uso fika siku kenda

Nimechoka na kuimba, nilipe na nitaenda


Mwezi umekamilika, hadi lini tasubiri?

Mwajiri waajibika, waniumiza kisiri

Hu ni ukweli hakika, moyoni waniathiri

Nimechoka na kuimba, nilipe na nitaenda


Nazivunja zangu sera, nizokuwa nimetenga

Nipe wangu mshahara, labda jumba tajenga

Nikuwapo na subira, waniona mi mjinga

Nimechoka na kuimba, nilipe na nitaenda


Wewe wacha zako pupa!, hivyo ndo waniambia

Njoo kesho nitakupa, na kikomo ushatia

Nijapo kile wanipa, nashindwa kukipangia

Nimechoka na kuimba, nilipe na nitaenda


Kazi hi nipo chagua, lijua tavumilia

Ila yanayotokea, naona kujiondoa

Mwajiri nakulilia, haki zangu natetea

Nimechoka na kuimba, nilipe na nitaenda


Mbona sasa wanyamaza?, kilio changu sikia

Haki zangu nauliza, mbona kazitupilia

Kwako wewe wala piza, nami nja navumilia

Nimechoka na kuimba, nilipe na nitaenda


Fuata zote sheria, zotengwa na serikali

Mwajiri u zingatia, haki zangu za awali

Maskini naumia, mana uchumi u ni ghali

Nimechoka na kuimba, nilipe na nitaenda.

@jephinternational



Share - Kilio Changu Mwajiriwa

Support this user by sending bitcoin - Learn more

0 comments

Be the first to comment!

This post is waiting for your feedback.
Share your thoughts and join the conversation.